The United Republic of Tanzania, President's Office Regional Administration and Local Goverment, Mbeya Region

Highlights and Resources

MKUU WA MKOA WA MBEYA AWAAGIZA WAKUU WA WILAYA KUTENGA SIKU YA KUSHUGHULIKIA KERO ZA WANANCHI.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amos Makalla amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wote wa Halmashauri za Mkoani Mbeya kutenga siku ya alhamisi kila wiki kuwa siku ya kushughulikia kero za wananchi. Mhe. Makalla ameyasema hayo wakati akiongea na wananchi kwenye mkutano wa hadhara kijiji cha Luhanga wilayani Mbarali.
“ Kila siku ya Alhamisi kuanzia saa 4-8 utakuwa ni muda wa Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi na Wataalam wa Halmashauri kukaa katika chumba cha Mikutano na kusikiliza kero za wananchi wa eneo husika ili kupunguza idadi za kero zinazoletwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambazo zinaweza kushughulikiwa wilayani”
Aidha, Mkuu wa Mkoa ameshauri kuanzisha madawati ya malalamiko kuanzia ngazi ya kata ili kuweka urahisi wa wananhi kushughulikia kero zao kuanzia ngazi ya kijiji, kata tarafa hadi ngazi ya wilaya kabla ya kufika ngazi ya Mkoa.
Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa amewataka wananchi wa Kijiji cha Luangwa kuacha tabia ya kuwaoza wasichana wadogo na badala yake wapewe fursa ya kujiendeleza kielimu. Amesema kuwa elimu ndio urithi unaodumu kutoka kwa wazazi hivyo wazazi wanatakiwa kuwekeza katika suala hilo.
Mhe. Makalla amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano imewekeza kuongeza idadi ya walimu ili shule ziwe na walimu wa kutosha. Pia amewataka Wakurugenzi kuhakikiksha kuwa walimu wanaoajiriwa wanapangiwa sehemu zenye upungufu mkubwa wa walimu hasa vijijini.